Tofauti kati ya wanaume na wanawake zinafaa kupunguzwa kwa kuwawezesha wanawake

Tofauti kati ya wanaume na wanawake zinafaa kupunguzwa kwa kuwawezesha wanawake

Kuna haja ya kuzitambua juhudi za wanawake katika jamii kwa minajili ya kuziimarisha na kuhakikisha wanafaidika kiuchumi na kuwawezesha kuchangia maendeleo ya taifa kwa jumla.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Kina Mama Wakulima (Association of Women in Agriculture) wanawake wanafanya mchango mkubwa kwenye jamii ila mchango huo hautambuliwi.

Mwenyekiti wa Shirika hilo Bi. Judy Matu anasema kuwawezesha wanawake pia kutapunguza visa vya dhuluma dhidi yao na kupunguza tofauti za kiuchumi zilizopo kati ya wanaume na wanawake.

Matu ameyasema haya katika siku ya kuzindua mradi wa kuwainua kina mama kiuchumi kwa jina We-Care utakaotekelezea katika kaunti ya Kitui.

Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano na shirika la kimataifa lisilo kiserikali Oxfam Kenya na unanuia kujenga uwezo wa kina mama kujiinua kifedha na kuwawezesha kuimarisha mchango wao katika jamii.

Covid-19 imechangia umaskini


Kwa mujibu wa Bi Matu mradi huo unafanyika wakati ambapo tofauti kati ya wanawake na wanaume zimeongezeka kutokana na janga la Covid-19 huku umaskini miongoni mwa wanawake ukiongezeka.

Shirika pia linataka kina mama wa nyanjani kusaidiwa kuimarisha mbinu zao za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kufunzwa jinsi ya kufanya kilimo bora, usalama wa chakula na udhibiti wa rasilmali.

Utafiti wa Shirika la Chakula na Kilimo duniani FAO unaonyesha kuwa iwapo wanawake wangekuwa na nafasi sawa ya kufikia rasilmali kama wanaume idadi ya watu wanaokabiliwa na tisho la baa la njaa ingepungua kwa zaidi ya watu milioni 100.

Mradi huo pia unaanzishwa wakati ambapo mahakama moja mjini Nairobi iliamua kuwa wanawake wanastahili kufidiwa kutokana na mchango wao wanaofanya katika familia.

Jaji Teresia Matheka aliamua kuwa kazi ya kuwa mke inafaa kutambulia kama ajira rasmi na inastahili kulipwa mshahara

Matheka ambaye alikua anaamua katika kesi moja ya utata wa ndoa alisema kuwa ni makosa kwa mahakama kukosa kutambua mchango wa kina mama licha ya kuwa wanautoa muda wao mwingi kuhakikisha kuwa familia zinastawi.admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.