SEHEMU YA PILI: Nani atatunza Manguo, wakazi wavutana huku Manguo yaangamia

SEHEMU YA PILI: Nani atatunza Manguo, wakazi wavutana huku Manguo yaangamia

Kuna kulaumiana kwingi huku kinamasi cha Manguo kikiendelea kudidimia. Katika sehemu hii ya pili, tunaangazia wamiliki ardhi, wachafuzi na wale wanaofanya jitihada za kuokoa Manguo.

NA STEVE MOKAYA
MPIGA PICHA: GORDWIN ODHIAMBO


Mwandishi shupavu wa fasihi, Ngugi wa Thiong’o, 83, anakumbuka Manguo kutoka utotoni kama “mahali pazuri ajabu penye miti, vichaka na ndege.” Ingawa baadhi ya uzuri huo ungalipo, huenda usidumu milele.
Kinamasi hiki kilichoko katika nyanda za juu za katikati mwa Kenya kinazidi kuzorota kwa kasi sana.
Katika msimu wa kiangazi, maji yake hupungua sana, na wakati wa msimu wa mvua, mafuriko yake hujaza nyumba za watu. Haishii hapo. Mafuriko hayo pia hutishia barabara kuu ya Nairobi-Nakuru, iliyo karibu.
Vyanzo vya matatizo ya Manguo ni vingi, ila kikubwa zaidi ni ujenzi wa nyumba na kilimo katika mkondo wa maji ya kinamasi. Wengi wa watazamaji wanasema kuwa itakuwa vigumu kusuluhisha tatizo hili, kwa vile sehemu kubwa ya kinamasi iko chini ya umiliki binafsi.
Waithaka Kang’ethe, katibu wa Muungano wa wamiliki mashamba wa Manguo, alisema kuwa wako tayari kuondoka sehemu hiyo, ili kutoa nafasi ya uhifadhi wa kinamasi hicho, ila sharti walipwe fidia na serikali.
“Tuko watu sabini, wenye vyeti halali vya mashamba. Mashamba yetu yana jumla ya ekari 12 kwenye kinamasi hiki. Ikiwa serikali itatulipa fidia, tuko tayari kuondoka kutoka sehemu hii. Na kwa vyovyote vile, sisi ndio watu wa kwanza tulioanzisha mikakati ya utunzi wa sehemu hii,” alisema.

14 Septemba 2021: Mifugo wanakula nyasi kando ya kinamasi cha Manguo

Mugo Kimani, waziri wa ardhi katika serikali ya Kaunti ya Kiambu, alisema kuwa ofisi yake iko tayari kwa mazungumzo. Hata hivyo, alionyesha ati ati kwa madai ya muungano wa wamilki mashamba. “Sijawahi kusikia mtu yeyote akisema kuwa sehemu ya Manguo ni yake. Nijuavyo mimi, hakuna aliye na cheti cha umiliki ardhi ya kinamasi cha Manguo, kwa sababu ni kitega uchumi asilia, na vitega uchumi vyote vya asili ni mali ya umma,” alisema.
“Hata hivyo, ikiwa watakuja kwenye ofisi yangu na tuhakikishe kuwa vyeti vyao ni halali, basi tunaweza tukajadili lipi la kufanywa. Lakini tena, ni vizuri kuzingatia kuwa kuna ufisadi, na yeyote anaweza kutengeneza cheti chochote ghushi. Ndio maana tunahitaji kushughulikia jambo hili katika ushirika na wizara ya ardhi ya serikali ya kitaifa,” Kimani alisema.

VYETI VYETU VYA MASHAMBA SIO GHUSHI


Kang’ethe alifutilia mbali madai kuwa walipata vyeti vyao kwa njia isiyo halali.
“Ardhi hii iligawanywa na kupewa wazazi wetu mwaka wa 1958. Wakati huo, ulafi wa ardhi hata hukuwa kwa sababu kulikuwa na ardhi nyingi ya kutosha kila mtu. Mbali na hayo, hata Kamati ya Manispaa ya Limuru inatambua kuwa kinamasi hiki kiko chini ya umiliki binafsi. Hiyo sio siri,” alisema.

Waithaka Kang’ethe, katibu wa chama cha wamiliki mashamba ya Manguo.

Kang’ethe alisema kuwa serikali ya ukoloni ya wakati huo iligawa sehemu ya Manguo na kutoa vyeti vya umilki ardhi mwaka wa 1959. Alituonyesha nakala ya manispaa ya Limuru ya mwaka wa 2009 iliyoashiria kuwa ardhi ya kinamasi hicho iligawa kwa vipande 200 vilivyomilikiwa na watu binafsi.
Karuga Ngigi, mbunge wa bunge la serikali ya kaunti ya Kiambu, anahisi kuwa serikali yapaswa kufanya zaidi iwapo inatilia maanani suala la kuhifadhi Manguo.
“Suala la ardhi

huwa na uzito mkubwa. Isitoshe, kinamasi hicho kina umuhimu mkubwa kwa watu wa Limuru. Serikali yafaa itafute mbinu za ushirikiano kati ya umma na sekta binafsi ili kufufua na kutunza Manguo.
Na kwa wale wanaodhani kuwa watamiliki sehemu ya kinamasi hicho milele wanajidanganya wenyewe, kwa sababu kitajitunza chenyewe, kwa mafuriko ambayo yatawafurusha.
“Hiyo ndiyo imekuwa hali kwa muda mrefu sana. Na maji kwenye kinamasi hicho hayawezi kuondolewa yote, iwapo wnafikiria kuwa wanaweza kufanya hilo,” Ngigi alisema.

KUJARIBU KUOKOA MANGUO

Wanjiru Mukoma, mtaalamu aliyebobea katika shughuli za kijamii na mwanzilsihi wa Marafiki wa Manguo, alisema kuwa walikuwa wamejitolea kuweka mikakati itakayopelekea kuokolewa na kuhifadhiwa kwa kinamasi cha Manguo.
Alisema kuwa walikuwa wameongea na muungano wa wamiliki ardhi wa Manguo, na kuwaeleza malengo yao.
“Hilo ndilo lilikuwa kundi gumu zaidi kushawishi, kwa sababu lina watu walioishi hapa kwa zaidi ya miaka themanini, na hivyo wanadai kuwa wakazi na wamiliki halisi wa ardhi izungukayo kinamasi hiki,” alisema.
Alisema kuwa pindi tu washiriki wa muungano huo walipoelewa kuwa lengo la Marafiki wa Manguo sio kuhusu umiliki, waliwakubali haraka na kubariki mipango yao ya kuhifadhi kinamasi hicho.
Mbali na wamiliki mashamba, Mbira Mukoma, ambaye ni katibu wa Marafiki wa Manguo, ana wasiwasi kuhusu mipango ya serikali ya kupanua barabara kuu ya Nairobi-Nakuru iwe na barabara nne.
“Tayari, barabara hii inahitilafiana na kinamasi hiki, kwa sababu yeyote anaweza kuona kuwa mwanzo kabisa ilijengwa ikipita kati kati mwa kinamasi chenyewe. Mipango hiyo ya upanuzi inamaanisha kuwa barabara itachukua sehemu nyingine ya Manguo,” alisema.
Hata hivyo, Charles Njogu, ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano katika Mamlaka ya Barabara Kuu za Kenya (KeNHA), alifutilianmbali wasiwasi huo. “Tuko katika hatua za ununuzi. Hata muundo wa barabara wenyewe hujachorwa. Kwa sasa, siwezi kuzungumzia kuhusu athari za upanuzi huo kwa mazingira. Hilo tutalizungumzia baada ya muundo wa barabara kuwa tayari,” alisema.

KERO LA UCHAFUZI


Marafiki wa Manguo pia wanataka kukomesha uchafuzi wa Manguo. Wanaamini kuwa kitakapookolewa, kinamasi cha Manguo kitaweza kupunguza baadhi ya athari zilizosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi. Mbira alisema kuwa kukomesha uchafuzi pia kutafanikisha shughuli ya ujenzi wa kituo cha mila na tamaduni katika sehemu hiyo.
Tayari, Marafiki hao wameomba msaada wa mwandishi maarufu, Ngugi wa Thiong’o. Ngugi alikulia katika eneo hili, na ako na nyumba karibu na Manguo.
Mwandishi huyo sasa anaishi nchini Marekani, ila bado anajali kuhusu nchi ya Kenya, kuhusu Limuru na kinamasi cha Manguo haswa kwa sababu ni mazingira ya ujana wake.
“Najua kuwa familia ya Profesa imekuwa na wazo hilo la kujenga kituo cha mila na tamaduni. Tunaweza kushirikiana na wao kufanikisha mradi huo, utakaofaidi jamii na kizazi kijacho. Nyumba yake iko karibu na hapa, takriban mita mia mbili kutoka kwenye kinamasi hiki,” alisema.
Manguo ni maudhui kuu ya riwaya ya binti ya Profesa Ngugi, Wanjiku wa Ngugi. Riwaya hiyo, iitwayo Seasons in Hippoland, ilikuwa ichapishwe mwezi Oktoba.
Profesa Ngugi alitoa usemi wake kwa barua pepe na kusema: “Kama watoto, tulikuwa tunaogelea kwenye maji ya Manguo. Raha.” Alikaribisha jitihada za Marafiki wa Manguo.
Hata hivyo, analaumu kampuni ya viatu ya Bata, kwa uharibifu na kuweka sumu katika kinamasi cha Manguo.
“Kwa miaka mingi, uchafu kutoka kwa mashine zake ulikuwa unamwagwa katika kinamasi cha Manguo. Hii ilikuwa ni sumu tupu. Kufikia wakati kampuni hiyo iliacha kufanya hivyo, muda ulikuwa umeenda na maovu kutendeka,” alisema. Kadhalika, aliongeza kuwa kampuni hiyo inafaa kushtakiwa, kwa uharibifu wa Manguo.
Hata hivyo, Bata ilisema kuwa madai ya Profesa Ngugi hayana ukweli.
John Ngoru, ambaye ni afisa wa maswala ya wafanyakazi katika kanda ya Afrika, alisema kuwa haiwezekani kumwaga uchafu kuelekea juu ya mlima: “Kinamasi hicho kiko kwenye sehemu iliyoinuka, ukilinganisha na mahali kiwanda chetu kiko. Iweje basi, tumwage uchafu juu ya mlima?”
Aliongeza kuwa kiwanda chao kimekuwa katika sehemu iyo hiyo ya hekta 65, iliyoko takriban kilomita moja kusini mwa Manguo, tangu kuasisiwa kwake mjini Limuru mwaka wa 1946.
Ngoru alikiri kuwa kwa miaka mingi, kiwanda hicho kilikuwa kinatoa uvundo mkali ambao ulikuwa umesambaa katika mji wa Limuru. Hata hivyo, alisema kuwa uvundo huo uliisha miaka 20 iliyopita, wakati kampuni hiyo ilianza kutumia ngozi iliyotibiwa.
“Sasa shughuli yetu ni safi na rafiki kwa mazingira. Kadhalika, tunao mkondo wetu wa kutibu na kuhifadhi uchafu wa kiwanda chetu,” alisema. Aliongeza kuwa shughuli zao hupekuliwa na kukaguliwa kila mwaka.
Ngoru aliongeza kuwa sio Bata inafaa kulaumiwa bali watu walioingilia sehemu ya kinamasi hicho na kujenga. Alisema kuwa serikali yafaa kushughulikia suala hilo la umiliki wa ardhi ya Manguo.
Aliongeza kuwa kampuni ya Bata huenda ikasikiza maombi ya msaada wowote kutoka kwa Marafiki wa Manguo.
Hata hivyo, kulingana na baadhi ya wakazi wa Limuru, Bata sio chanzo pekee cha uchafuzi. Walisema kuwa kichinjio kilichoko kando ya kinamasi kimekuwa kikichafua Manguo na kuua baadhi ya wanyama waishio humo.

14 Septemba 2021: KIchinjio kilichoko kando ya kinamasi cha Manguo. Kwa wengi kichinjio hiki kinachangia katika uchafuzi wa mazingira.

Meneja wa kichinjio hicho kiitwacho Bahati, Alex Mburu Kang’ethe (Hakuna uhusiano na katibu wa muungano wa wamiliki ardhi) alifutilia mbali madai haya.
“Tunachinja ng’ombe sitini kwa siku, na uchafu wetu husimamiwa vizuri. Tuko na mapipa matatu ya uchafu ardhini, tunaposafisha na kutibu uchafu kabla ya kuusukuma kwenye mkondo wa taka. Fauka ya hayo, tumepewa vibali na mamlaka zote zifaazo za serikali, zikiwemo kitengo cha mifugo na mamlaka ya kitaifa ya mazingira (NEMA) ili kufanya shughuli katika kichinjio hiki,” alisema.
NEMA ilikiri kuwa kichinjio hicho ambacho kimekuwa kikiendesha shughuli zake kwa zaidi ya miaka ishirini, kimezingatia sheria zote zilizowekwa. “Vinginevyo, kingekuwa kimefungwa kitambo sana,” mamlaka hiyo ilisema.

UMILIKI WA ARDHI NA SHIDA YA MAJI

Wanjiru anaamini kuwa iwapo maji kutoka kwenye kinamasi hicho yanaweza kutunzwa na kuhifadhiwa vyema, yanaweza kupunguza njaa katika eneo hilo.
“Tunashuhudia mafuriko na ukame, kinyume na awali. Katika miezi mingine, kinamasi hiki karibu hukauka kabisa. Kipindi hicho, eneo hili hushuhudia uhaba wa chakula. Ndiyo maana tunataka kufufua maji haya, ili wakazi wayatumie kufanya kilimo cha unyunyuzaji, na pia kutengeneza ajira kwa vijana wengi wasio na kazi,” alisema.
Kikundi hicho kimekuwa na mikutano ya mafunzo kuhusu utunzi na uhifadhi wa maji na mamlaka ya rasilmali za maji (WRA).
John Kinyanjui, meneja wa uangalizi na makadirio katika mamlaka hiyo alisema kuwa kulinda kinamasi cha Manguo kumekuwa jambo gumu kwa miaka mingi sasa, kwa sababu ywa watu wengi wanaodai kumiliki sehemu hiyo.
Hata hivyo, mpango mpya unaandaliwa ili kunyoosha mambo.
“Sasa tunapanga kudhibiti kile kinachoweza kufanywa na wale walio na vyeti vya ardhi kwenye kinamasi hicho, kwa sababu ni vigumu kuwa na nguvu za kudhibiti kila kitu huko. Tutakuwa na mazungumzo na wao ili tuwaeleze kuhusu mambo ambayo hataweza kufanya. Mambo hayo ni kama kuendeleza shughuli yoyote ya kilimo, kukata miti asili, kujenga, kupanda miti na kumwaga uchafu katika sehemu hiyo.
“Iwapo watapinga mpango huo, basi itatubidi tuhusishe tume ya kitaifa ya ardhi (NLC), ili kusuluhisha kitendawili hiki cha umiliki wa ardhi ya kinamasi cha Manguo,” alisema.
“Kuna vinamasi na mabwawa mengi katika maeneo ya Kiambu na Nairobi, ambazo ardhi yao imegawawanywa miongoni mwa wakazi. Lakini watu hao huishia kufurushwa na vinamasi na mabwawa hayo, wakati yanafurika. Watu wanafaa kujua kuwa kuna zaidi ya ujenzi na kilimo katika sehemu hizi. Vinamasi vina umuhimu mkubwa vinapoachwa jinsi vilivyo, pasi na kuingilia na yeyote. Labda, kile wanaweza wakafanya ni kuvifanya viwe vivutio vya watalii,” alisema.

VISIMA NA KUFUNGWA


Caroline Muriuki, afisa mkuu wa NEMA anayesimamia vinamasi anajuta kuwa mamlaka ya NEMA ina usemi mdogo sana juu ya Manguo. Aliongeza kuwa kuchimbwa kwa visima vya maji katika kinamasi hicho kuliharibu hali hiyo zaidi.
“Manguo imekabiliwa na umiliki kadhaa wa ardhi ulio binafsi, na wamiliki hao wana vyeti vya umiliki. Hivyo, inakuwa ni vugumu kwetu kujihusisha na katika shughuli za Manguo. Isitoshe, kampuni ya maji ya Limuru inavuta maji mengi kuliko inavyostahili kutoka kwenye kinamasi hicho. Ndio maana Manguo inakabiliwa na athari ya kukauka kabisa,” alisema.
Afisa wa kiwango cha juu kutoka kwenye kampuni ya maji ya Limuru alipinga madai hauo. “Kampuni yetu ina visima sita. Vinne viko karibu na kinamasi cha Manguo, na vinatoa maji 15-cubic metres kwa saa moja. Isitoshe, mashine zetu hazivuti maji moja kwa moja kutoka kwenye kinamasi, mbali mita mia mbili ardhini. Kwa hivyo, huwezi kusema kuwa tunatoa maji mengi kuliko inavyostahili,” alisema.
John Kinyanjui alikubaliana na maelezo haya. Alisema kuwa visima hivyo hupiga maji kutoka chini ardhini, wala sio kutoka kwenye kinamasi. “Fauka ya hayo, tunadhibiti viwango vya maji ambayo yanaweza kuvutwa kutoka chini ya ardhi. Hakuna jambo kama kuvuta maji kuliko inavyofaa,” alisema.


1 Octoba 2021: Kampuni ya maji ya sehemu hii ikichimba bomba la maji karibu na kinamasi

Hata hivyo, John Mironga, ambaye ni mtafiti wa maisha kwenye vinamasi, na mhadhiri mkuu katika chuo kikuu cha Egerton, anapinga maelezo haya.
“Kampuni hiyo inajua mbona walichimba visima karibu na kinamasi hicho. Ni kwa sababu wanajua kuwa meza ya maji huwa karibu na ardhi kwenye vinamasi, na hivyo ni rahisi kupata maji. Fauka ya hayo, maji zaidi ya kinamasi huingia ardhini. Na hayo ndiyo majiambayo kampuni hiyo inayavuta,” alisema.
“Ukipita kwenye barabara kuu ya Nairobui-Nakuru, utaona wazi kuwa Manguo karibu inakuwa kama uwanja wa michezo. Ama kwa yakini, watu hucheza huko, kwa sababu kumekauka. Lakini hali haikuwa hivyo awali. Hata wakatae, visima vyao vimechangia kwa kudidimia kwa maji ya Manguo,” alisema.
Mironga alionya kuwa kufungwa kwa vinamasi huumiza viumbe waishio humo, na kuathiri viwango vya maji.
“Vinamasi huwa na maji safi. Unavyofunga mikondo yake za kutolea maji, maji hukaa humo kwa zaidi ya inavyostahili. Maji yanapofungiwa kwa muda mrefu bila kutoka, viwango vyake vya uchachu vinapanda. Maji hayo huacha kuwa freshi na na hivyo kuathiri viumbe waishio humo,” alisema.

1 Octoba 2021: Kinamasi cha Manguo kinakabiliwa na hatari za kusumbuliwa na kuchafuliwa na idadi kubwa ya watu wengi wanaoishi hapo pamoa na kuwa karibu na mji wa Limuru na barabara kuu ya Nairobi kuelekea Nakuru .

Mbira Mukoma, katibu wa Marafiki wa Manguo, alisema kuwa iwapo mzozo huo hautasuluhishwa, uhasama na athari kati ya visima na kinamasi ungesalia.
“Kinamasi kimekuwa hapa tangu jadi. Visima navyo vimechimbwa tu juzi, na vikachimbwa pasipofaa. Ilimradi visima hivi vingalipo, viwango vya maji ya kinamasi vitazidi kudhibitishwa, ili maji yasije yakafunika mashine za kupiga maji haya . Na hilo ni kosa. Natumai kuwa kampuni itatafuta njia ya kuhamisha mashine zao za kupiga maji kutoka kwenye kinamasi, na wazihamishie shemu za juu kidogo, ili maji ya Manguo yajae vile inavyofaa,” alisema.
“Iwapo wananchi wangejua umuhimu wa vinamasi maishani na katika kuleta maji, wangekuwa na ari zaidi ya kuvilinda. Vinamasi vya nyanda za juu aghalabu huwa katika sehemu ya uzalishaji mkuu, na yenye mvua nyingi. Kwa hivyo, vinahifadhi mengi ya maji ya mvua kunaponyesha. Maji haya yanaweza kutumika mbeleni, nyakati za kiangazi. Isitoshe, vinamasi hivi hudhibiti mafuriko, hasa katika sehemu za nyanda za chini, kwa kuweka maji mengi ya mvua,” Muriuki alisema.
Aliongeza kuwa Kenya iko na sheria nyingi na pana kuhusu uhifadhi wa vinamasi, na hahiitaji sheria zingine.
“Ama kwa yakini, Uganda na Rwanda zinatumia sheria zetu na zinafanya vyema kuliko sisi. Kwa hivyo, hitaji letu kuu ni uhamasishaji wa umma ili uweze kufanya kile kinachofaa,” alisema.
Mironga alisema kuwa vinamasi ni vya muhimu sana katika maisha na vinapaswa kulindwa kwa vyovyote vile.
“Vinamasi ni kama maini. Vinasafisha uchafu wote huingia humo: wa hewa, maji maji na kadhalika. Vinamasi vimechukua sehemu asilimia sita ya ulimwengu. Zaidi ya hayo, vinavuta asilimia ishirini ya kaboni ya dunia, na hivyo kudhibiti joto la dunia na mabadiliko ya tabia nchi. Taifa la Kenya lina vinamasi vya bara vyenye jumla ya ukubwa hekta zaidi ya milioni 2,” alisema.
Mironga alisema kuwa Manguo iko kwenye athari kubwa kuliko vinamasi vingine, kwa sababu ya sehemu iliko.
“Iko kwenye barabara kuu ya Nairobi-Nakuru, na kando ya mji wa Limuru. Hivyo, ni rahisi sana kufikiwa. Yeyote apitayo sehemu ile huiona kama sehemu nzuri yenye uwezo mkubwa wa kukua na kufanya maendeleo. Shinikizo la idadi ya watu kutoka Nairobi na Limuru linaiweka Manguo katika hatari ya kuangamizwa kabisa,” alisema.
Jamii na kampuni ya maji ya Limuru zinafaa kushirikiana kutunza Manguo, alisema.
“Kampuni hiyo ya maji hupata pesa nyingi sana kutokana na maji inayotoa kwenye kinamasi. Ama kweli, inafaa itumie baadhi ya faida hiyo kutunza kinamasi cha Manguo.”

Steve Mokaya ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika shahada ya taaluma ya uanahabari jijini Mombasa, Kenya. Makala hii iliandikwa kwa uelekezi wa shirika la habari za mazingira la Roving Reporters. Makala hii ni mojawapo ya mradi wa ripoti za habari kuhusu mazingira, uliofadhiliwa na shirika la Internews Earth Journalism Network. Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na shirika la habari la New Frame, la Afrika Kusini.

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.