SEHEMU YA KWANZA: Nani atatunza Manguo, wakazi wavutana huku Manguo yaangamia

SEHEMU YA KWANZA: Nani atatunza Manguo, wakazi wavutana huku Manguo yaangamia

Kinamasi cha Manguo kilichoko  eneo la Limuru kinaangamia pole pole, kwa sababu ya shughuli za wakazi na kutelekezwa na mashirika ya serikali. Lakini je, mikakati mipya iliyowekwa inaweza kuokoa Manguo na rasilmali yake ya wanyamapori?

NA STEVE MOKAYA
MPIGA PICHA: GORDWIN ODHIAMBO

This image has an empty alt attribute; its file name is Manguo-aa-1024x683.jpg
1 Octoba 2021: Waithaka Kang’ethe, (72) Katibu wa chama cha wamiliki Mashamba wa Manguo kilichoanzishwa mwaka wa 2008 kujaribu kuhifadhi kinamasi na kulinda haki za wanaodai kumiliki sehemu ya kinamasi hicho.

Bata wanaogoela kwenye kinamasi cha Manguo, huku sauti za kuvutia za ndege zikijaa hewani. Ng’ombe, kondoo na mbuzi wanakula kwenye nyasi ya kijani iliyoko kando kando mwa maji. Kwa upande mwingine, vijana wanakata nyasi kupelekea mifugo nyumbani. Ni hali yenye utulivu, ambayo inasumbuliwa mara moja moja na sauti ya magari yanayopita kwenye barabara kuu ya kuelekea Nairobi karibu.
Hata hivyo, hali sio shwari kwenye kinamasi hiki kilichoko karibu na mji wa Limuru, ulioko kilomita 45 kutoka mji mkuu, Nairobi na chenye ukubwa wa takriban mita mia nne, elfu themanini na tano mraba (485,000 m²).
Katikati mwa kinamasi hiki kuna kisiwa kidogo ambacho ukubwa wake pengine ni nusu ya uwanja wa kandanda. Mianzi mingi iliyokuwepo sasa haiko. Baadhi ya watu wanalaumu ukataji mkubwa wa miti hii kama chanzo cha kudidimia kwake. Mianzi ni kifaaa muhimu katika ujenzi wa nyumba asilia.
Wazee wa hapa wanasema kuwa viwango vya maji kwenye kinanmasi cha Manguo vinapungua nyakati za kiangazi, kinyume na kitambo. Kando kando mwa Manguo, miti ya mikaratusi almaarufu kama eucalyptus kwa kizungu, na ivutayo maji mengi, inazidi kukua kila uchao.
Utafiti wa Shirika la Makavazi nchini kuhusu aina ya ndege wanaopatikana hapa ulirekodi zaidi ya aina 50 za nyuni. Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, wakereketwa wa kutazama ndege wamekuwa wakiona ndege wachache, kulingana na Waithaka Kang’ethe, ambaye amekaa katika eneo hili siku zote za maisha yake. “Watoto wachezao hapa huchukua mayai kutoka kwenye viota,”alisema.
Titus Imboma, mjuzi wa ndege kutoka kwenye Shirika la Makavazi nchini, hashtushwi kuwa idadi ya ndege inapungua, na alitoa usemi mkali: “Unatarajia nini ukiruhusu uwundaji na uingiliaji wa sehemu hiyo? Watu wamechangia pakubwa katika kupungua kwa idadi ya ndege katika kinamasi cha Manguo. Wanawinda mayai na hata kujaribu kuvuga baadhi ya ndege hao. Wanakata miti na nyasi, ambayo ni makazi ya ndege,” alisema huku akiongeza kuwa elimu na kutengenezwa kwa nafasi za ajira za utalii huenda ikasaidia.
Wanyama wakubwa, kama vile viboko walihama sehemu hii zaidi ya kizazi kilichopita.
Wengine wanalaumu kupungua kwa ndege na maovu mengine yaliyopo Manguo kwa mabadiliko ya tabia nchi, ila mengi ya madhara haya yamesababishwa na binadamu.

WATU NDIO SHIDA

Kampuni ya maji katika eneo hili imenyooshewa kidole cha lawama kwa kuchukua maji mengi kutoka Manguo, ila imepinga lawama hizo. Pia wajenzi binafsi wamejenga nyumba katika mikondo ya maji ya kinamasi, miti asilia imekatwa na mipya kupandwa, kilimo kinaendelezwa kwenye sehemu ya maji ya Manguo, na mipango ya kupanua barabara ya Nairobi-Nakuru, iliyo karibu, inaendelea.
Njia asilia za kinamasi za kutolea maji zaidi zimefungwa, zikafunguliwa na kisha zikafungwa tena, na kupelekea mafuriko nyakati za mvua nyingi. Wapinzani wanalaumu mashirika ya serikali na viongozi kwa kutochukua hatua kwa sababu ya kura kuu zijazo Agosti mwaka ujao.
Umiliki binafsi wa baadhi ya sehemu za Manguo, na tuhuma za ufisadi katika zoezi la kutoa vyeti vya mashamba yaliyo karibu zinachanganya mambo zaidi, na kurudisha nyuma mikakati ya utunzaji. Ni mchanganyiko mkubwa wa maslahi kinzani, ambao umekataa kukumbatia suluhu, na unaoashiria vikwazo vilivyopo katika mikakati ya kulinda vinamasi vingine kwingineko nchini Kenya.

This image has an empty alt attribute; its file name is Manguo-aaa-1024x681.jpg
1 October 2021: Hoteli karibu na Manguo kuwashughulikia watalii. Wamiliki wanasema idadi ya watalii imepungua katika siku za hivi karibuni.

“Manguo ilikuwa na maji mwaka mzima, ila sasa viwango vyake vinapungua kiasi kwamba karibu panakauka kabisa,” alisema Kang’ethe mwenye umri wa miaka 72. Yeye ndiye katibu wa Muungano wa Wamilki Mashamba ya Manguo (MWMM), ulioanzishwa mwaka 2008 kuhifadhi kinamasi hiki na kulinda maslahi ya washiriki wa kikundi hiki.
Alisema kuwa serikali ya Uholanzi ilitoa shilingi milioni 1.2, iliyotumiwa kujenga ukuta wa kinamasi Manguo. Ila baada ya muda, mradi huo ulianguka kwa vile washiriki 70 wa muungano huo walichoka kulinda mchana na usiku.
“Ndipo uharibifu ukaja. Watu walitoroka na sehemu za ua, na wakaharibu minara ya ulinzi.”

HAKUNA USAIDIZI WA SERIKALI

Kang’ethe analaumu serikali ya Kenya. “Serikali ya Uholanzi ilisema kuwa ingeendelea kutusaidia kwa fedha iwapo Kenya ingesaidia pia. Tumeandika nakala nyingi kwa Manispaa ya Limuru tukiomba usaidizi wa fedha lakini wapi! Nakala ya mwisho kutumwa ilikuwa Agosti mwaka jana. Kama kawaida, hakuna lolote lililofanywa,” alisema.
Tuliongea na ubalozi wa Uholanzi jijini Nairobi kwa usemi, ila hadi wakati wa uchapishaji, hakukuwa na jibu.
Kang’ethe alisema kuwa jitihada za muungano wao za awali zilileta pesa fulani. “Tulikiwa tunalipisha watalii kuona ndege huku. Fauka ya hayo, tulikuwa tunalipisha wakazi kwa kulisha mifugo wao kwenye kinamasi. Hivyo, tulikuwa tumepata shilingi laki tatu wakati ambapo tuliacha shughuli hiyo. Pesa hizo ziko kwenye akaunti ya benki ya muungano wetu. Tunatarjia kupata msaada zaidi wa pesa siku moja, ili turejelee jitihada zetu za awali.”

This image has an empty alt attribute; its file name is Manguo-aaaa-1024x682.jpg
14 September 2021: Mojawapo wa bomba la maji lililoko kwenye kinamasi cha Manguo. Mwaka wa 2020 bomba hili lilifunika na maji ya mafuriko na kusababisha uhaba mkubwa wa maji katika mji wa Limuru.

Joseph Munyaka, mmoja wa washiriki wa muungano huo, alijenga hoteli karibu na Manguo, katika sehemu iliyoinuka. “Walianza kuja kunywa vinywaji na kutumia vyumba vya usafi. Kadhalika, wangepiga picha kutoka sehemu hii ya juu,” alisema.
Ila baada ya muda, biashara ya utalii ilididimia na leo hii, hoteli hiyo imesalia yenye vumbi na legelege. Viti katika sehemu ya juu ya kutazamia kinamasi na ndege vimevunjika na mavi ya ndege yametapakaa kote kote. Ni sehemu ya chini pekee inayotumika kwa sasa, na haswa kwa kuuzia bia kwa wazee wa sehemu hiyo tu.
Ingali kitendawili kuhusu ni nani wa kulaumiwa kwa kudidimia kwa kinamasi cha Manguo, na ni nani anayefaaa kugharamia gharama ya ufufuzi wake.

KUNA USHINDI KWINGINEKO

Jitihada za kurekebisha vinamasi vingine kwinginekeo katika nyanda za juu za Kenya zimepata ufanisi wa kiwango fulani, na kuashiria kile ambacho hatua za wananchi kinaweza kufanya. Katika kinamasi cha Ondiri kilichoko karibu na Nairobi, ua mkuu umejengwa, uchafuzi kuzuiliwa, shemu za kutembea zimetengenezwa na miti asili kupandwa na Marafiki wa Ondiri.
Na sasa, Manguo pia inao washirika wenye ari ya kuihifadhi.
Wanjiru Mukoma, aliyefanya kazi na mashirika ya kijamii na yasiyo ya serikali kwa miaka mingi, amefanya juhudi za kufufua Manguo kuwa azma yake. Manguo iko takriban mita mia tatu kutoka kwake. Ameshirikiana na wakazi wengine na kuunda kundi la Marafiki wa Manguo.
“Tunaweza kufufua kile ambacho kundi la kwanza lilifanya, na hata tufanye vizuri zaidi, na tufanye Manguo kuwa sehemu kubwa ya utalii na kitega uchumi,” Wanjiru alisema. Alisema kuwa kinamasi hicho kinaweza kuvutia watalii wengi, kwa sababu kiko kwenye barabara inayoelekea mbuga tajika ya Maasai Mara kutoka Nairobi.

This image has an empty alt attribute; its file name is Manguo-aaaaa-1024x683.jpg
14 September 2021: Bomba la maji machafu lililojengwa karibu na kinamasi cha Manguo na kuhatarisha maji ya kinamasi

Kikundi chao kina washiriki kumi, ila wanatarajia kuongeza wengine ishirini. Hii itawawezesha kusajili Marafiki wa Manguo kama shirika la kijamii, na hivyo kufungua milango ya kuchangisha pesa. Kwa sasa, washiriki hao wanagharimia shughuli zao kwa pesa zao.
“Jambo la kutafuta pesa si kubwa vile. Hilo tutashughulikia. Ila lazima kwanza tusajili kikundi chetu, na tuwe na nakala rasmi, ndio hata wa kutoa misaada waweze kuwa na ujasili wa kutupa fedha,” alisema.
Kikundi hicho kiliundwa muda mfupi baada ya mafuriko kuharibu makazi ya familia ishirini mjini Limuru Mei mwaka 2020, wakati ambapo mvua nyingi zilifanya kinamasi hicho kujaa zaidi na kuvunja kingo zake. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, mafuriko hayo yalitishia kujaza barabara kuu ya Nakuru-Nairobi.

This image has an empty alt attribute; its file name is Manguo-aaaaaa-1024x682.jpg
14 Septemba 2021: Wakili Robert Githire alisema alishirikiana na kundi la wanawake kuzibua mikondo ya maji iliyofungwa na wamiliki wa ardhi wa sehemu hiyo.

MAELEZO YANAYOKINZANA

Karuga Ngigi, ambaye ni Mwakilishi wadi wa sehemu hiyo katika bunge la kaunti ya Kiambu, alisema kuwa mafuriko hayo yalifunika mashine ya kupiga maji ya kampuni ya Limuru Water, na hivyo kusababisha shida ya maji, ambayo iliathiri maelfu ya watu wategemao maji ya mfereji.
Wakati huo huo, kampuni ya umeme ya Kenya Power ilikata umeme katika eneo hilo, ili kuzuia janga kutokea.
“Shida hizo mbili (ukosefu wa maji na umeme) zilifanya watu kujitokeza barabarani kuzua rabsha kuonyesha ghadhabu yao, na kushinikiza kufunguliwa kwa njia za maji za kinamasi,” alisema Ngigi.
Ila David Kuria, waziri wa maji na mazingira katika serikali ya kaunti, alisema kuwa serikali ya kaunti iligundua kuwa kulikuwa na jambo na hivyo ikachukua hatua.
“Baadhi ya watu walikuwa wamefunga njia za maji ya Manguo kwa kumwaga mchanga ila tulituma tinga tinga zikaja zikautoa, na maji yakaanza kupita,” alisema. “Hakukuwa na rabsha hata.”
Ngigi hata hivyo, alaisema kuwa ni rabsha za wananchi ambazo zilisukuma serikali kuchukua hatua. “Hapo ndipo serikali ya kaunti ilipofungua sehemu zilizofungwa na kufungulia maji.”
Robert Githire, ambaye ni wakili kutoka Limuru anayepania kuwania kiti cha ubunge wa Limuru, alitoa maelezo tofauti pia. Alisema kuwa serikali ya kaunti ilijikokota kuchukua hatua, na hivyo ikamlazimu kuwaongoza wananchi kuandamana. Aliongeza kuwa wananchi walitumia sepetu na jembe kufungua sehemu za maji zilizofungwa.
“Wanawake saba kutoka Limuru walinijia na kunielezea shida zao. Hawakuwa na maji na hakuna jambo lililokuwa linafanywa. Nilienda nao na tukachimba mtaro. Maji yalianza kupita, japo pole pole,” alisema.
Hata hivyo, kitendo chao hakikudumu, kwa vile mjenzi binafsi aliyekuwa amezuia maji alienda na kufunga tena, kwa kutumia mchanga. Kwanza alikuwa anataka kujenga ukuta wa saruji, Githire alisema. “Hapo ndipo nilipoenda na watu kama hamsini hivi, na tukapafungua sawa sawa. Kisha tulikaa hapo kwa siku tano, tukichunga jitihada zetu zisiharibiwe tena.
“Mimi ni wakili kutoka kwa jamii, na nikifanyacho (kuwaongoza wananchi) ni kama kuwasaidia wanajamii. Wao hunijia popote wanapokuwa na shida inayowatatiza.”
Githire alidai kuwa alipewa hongo ya shilingi milioni moja aache kuwaongoza waandamanaji hao, ila akakataa.

UKUTA WA MZOZO

Wakati wa mafuriko ya awali, maji taka yalipitia katika mikondo ya maji ya kinamasi, na kufurika kwenye nyumba za kukodi za Patrick Muremwa.
Mwezi Mei mwaka huu, Muremwa alieleza sehemu alichokifanya. “Niliifunga kwa sababu wapangaji wangu walikuwa wanalalamika. Maji yalikuwa yameanza kuingia kwenye nyumba zao. Kwa bahati mbaya, wakati maji hayo yalikuja kwa nguvu zote, iliwabidi waondoke. Walitoka, na hawakurudi hadi tena. Nilipoteza mali nyingi katika biashara yangu. Haijakuwa rahisi kujaribu kuanza biashara nyingine.”
Alikiri kuweka ukuta mwezi wa Februari, na kufunga mkondo wa maji kabisa.
Mamlaka ya kitaifa ya kudhibiti mazingira (NEMA) imeweka alama ya kuuangusha ukuta huo, ila Muremwa anasema kuwa hashtushwi na hilo, wala hatautoa ukuta wake. “Siwezi kufanya kitu. Sitautoa. Niliuweka kulinda mali yangu dhidi ya uharibifu wa mafuriko, ikiwa yatatokea tena. Isitoshe, nahisi kuwa nasumbuliwa pasi sababu. Mbona ni mimi tu nasumbuliwa kutoka kila upande, na kunao watu wengine wengi waliojenga sehemu ya chini ya mkondo huu wa maji?”

14 Septemba 2021: Patrick Muremwa ni mmiliki wa nyumba karibu na kinamasi. Alijenga ukuta kwenye mkondo wa maji ili kuzuia maji kufikia nyumba za wateha wake. 

Carol Muriuki kutoka NEMA alifutilia mbali semi za Muremwa kuwa analengwa visivyo. “Anafaa kufanya sehemu yake. Anajua kuwa akifanyacho ni kinyume cha sheria. Sheria itamhukumu yeye kama mtu binafsi,” alisema.
Hata hivyo, Muriuki alikiri kuwa Muremwa, kama wengi waliojenga kwenye mkondo wa maji, wako na vyeti vya mashamba, ila akasema kuwa bado allichokuwa (Muremwa) akikifanya ni kinyume cha sheria. Aliongeza kuwa baada ya upekuzi na uchunguzi, NEMA ilikataza ujenzi wowote zaidi katika sehemu hiyo. “Ila yeye alikaidi na kujenga ukuta. Hapo ndipo alipokosea.”
Alisema kuwa NEMA ilikuwa kwenye mazungumzo na serikali ya kaunti. “Mazungumzo yanaendelea na najua itachukua muda kusuluhisha jambo hili. Tunaelekea kipindi cha uchaguzi na hakuna gavana atakayetaka watu wake kusumbuliwa, kwa sababu watawahitaji mwaka ujao kuwapigia kura. Tunahitaji mazingira rafiki ya kisiasa ili kutimiza mipango yetu. Kwa sababu hiyo, tutakuwa wavumilivu kidogo.”

KUKATWA KWA MAJI YA MFEREJI

Afisa wa juu katika kampuni ya Limuru Water alisema kuwa watu elfu tisa hutegemea kwa maji ya mfereji, na kuwa mafuriko ya Manguo yaliharibu mashine kubwa mbili, na kukata maji kwa watu elfu sita.
Afisa huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa maandamano ya wananchi yalisaidia sana kwa vile yalifanya serikali ichukue hatua. “Kama kampuni, hatukuwa na uwezo wa kufanya lolote kwa vile wafanyabiashara walikuwa wamefungia maji na kujenga nyumba.”
Alisema kuwa wananchi walitambua kiini cha ukosefu wa maji. “Walikaa huko siku yote hadi jioni wakati wa kafyu kuhakikisha kuwa mkondo wa maji hautafungwa tena. Ilichukua kama miezi matatu kabla ya maji kurejelea viwango vyake vya kawaida.”

14 September 2021: Ukuta ulioengwa na Patrick Muremwa uliokokwenye mkondo wa kutolea mai wa kinamsai cha Manguo

Maji yalipofunguliwa, Joseph Kahenya ambaye ni MCA wa wadi ya Limuru ya kati, alisema kuwa serikali ingewaondoa wote waliokuwa wamejenga kwenye sehemu ya maji. “Hii inamaanisha kuwa ikiwa kuna yeyote aliyejenga ama kuishi kwenye mkondo wa maji, jua kuwa serkali inakuja kuchukua sehemu yake,” Kahenya alinakiriwa na gazeti la The Star akisema.
Hata hivyo, zaidi ya mwaka umepita na hakuna hatua iliyochukuliwa. Wakazi wa nyumba zilizoko kwenye mkondo wa maji walirejea baada ya mfuriko kuisha. Hakuna aliyeondolewa wala hatua yoyote kuchukuliwa dhidi ya wenye nyumba.
Kahenya hakuwa amejibu wakati wa uchapishaji.
Ngigi, aliyechaguliwa katika tiketi ya Jubilee, ambacho ni chama kilichounda serikali, anailaumu serikali ya kaunti ya Kiambu. Alisema kuwa ilikuwa imefanya jitihada kidogo kuzuia mafuriko, ama kuwaondoa watu kutoka kwenye sehemu ya maji.
“Jambo pekee walilolifanya ni kuweka mikondo ya kupitisha maji, ila wakazi wa maeneo hayo bado wako tu,” alisema.
Kuria alisema kuwa umilki wa mashamba kwenye kinamasi cha Manguo ni shida ya tangu jadi.
“Kuna mzozo kuhusu umiliki wa mashamba yaliyo kwenye kinamasi. Ndio maana hatujaweka ua. Katika siku za nyuma, tumekuwa na mazungumzo na watu wanaodai kuwa wamilki wa sehemu hiyo, ila kwa bahati mbaya, hakuna suluhu lililopatikana.”
Alisema kuwa jitihada za kumaliza mzozo huo na kulinda kinamasi zingali zinaendelea. “Gavana wa kaunti pamoja na kamishana wa kaunti wameunda jopo la kushughulikia jambo hili. Tunazidi kungoja watupe njia za kufuata,” alisema.

Steve Mokaya ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika shahada ya taaluma ya uanahabari jijini Mombasa, Kenya. Makala haya yaliandikwa kwa uelekezi kutoka kwa shirika la habari za mazingira la Roving Reporters. Makala hii ni mojawapo ya mradi wa ripoti za habari kuhusu mazingira, uliofadhiliwa na shirika la Internews Earth Journalism Network. Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na Shirika la habari la New Frame, la Afrika Kusini.

 

 

 

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.