Mwandishi wa habari aasi kamera, akumbatia udaktari na unabii…

Mwandishi wa habari aasi kamera, akumbatia udaktari na unabii…

Sifa zake katika eneo la OJ kwenye vitongoji vya mji wa Ruiru kaunti ya Kiambu zimeenea kwa kasi ya moto wakati wa kiangazi.

Wengi wanamtambua kama tabibu aliyekolea kwa kutibu magonjwa aina mbalimbali kwa kutumia njia za kiasilia na mitishamba.

Ila sasa amepata amepata kazi mpya na anasema kuwa ameanza kuona maono ya kinabii.

Kang’ethe katika enzi zake kama mwandishi wa habari za televisheni. (Picha: Samwel Kang’ethe Facebook)

Samwel Kang’ethe maarufu kama Daktari Sammy ni mwandishi wa habari wa zamani ambaye aliwahi fanyia kazi kituo kimoja cha habari humu nchini kama mpiga mpicha na mwandishi wa habari za televisheni.

Ninapofika kumuona Daktari Samuel Israel Kang’ethe namkuta akiwa anatayarisha supu maalum inayotokana na mifupa ya ngamia ambayo anasema ni muhimu kwa watu ambao umri wao ni mkubwa na huenda labda wanasumbuliwa na viungo vya mwili.

“Supu hii pia ni muhimu kwa wale ambao huenda nguvu zao za kiume zimeanza kudidimia hasa kutokana na umri ama athari za marathi yanayotokana na uzee,” ananiambia huku akinionyesha chungu kinachotokota na harufu nzuri ya supu inatoka humo.

Kang’ethe katika enzi zake kama mwandishi wa habari za televisheni aliwahi tangamana na watu wa asilia mbalimbali. (Picha: Samwel Kang’ethe Facebook)


Kange’the ambaye sasa ni daktari anayetumia mbinu asilia anasema alipenda taaluma yake ya utabibu kutokana na ukweli kuwa mimea mingi ina virutubisho muhimu ambavyo vina tibu magonjwa mengi.

“Magonjwa mengi yanaweza kuepukika ikiwa tutatumia vyakula na matibabu ya kiasilia” ananiambia huku akinionyesha maktaba yake na nyaraka muhimu za kutambuliwa kama tabibu wa kutumia mbimu asilia.

Kwenye maktaba hii kuna vitabu kadhaa vinavyozungumzia utabibu wa kiasilia. Anasema vitabu hivi humsaidia katika kuonegza ujuzi wake katika kazi yake.

Kangethe amebobea katika kazi yake na baadhi ya mimea ambayo anatumia inatambuliwa na watafiti katika chuo kikuu cha Kenyatta.

Kang’ethe sasa anasema amekuwa nabii na maono yake yanastahili kukumbatiwa na wato waliolengwa. (Picha: Samwel Kang’ethe Facebook)

“Nilipeleka madawa aina kadhaa katika idara ya utafiti wa mimea asilia katika chuo kikuu hicho na wakaidhinisha kuwa inaweza kutibu” Kange’ethe anasema huku akinionyesha barua rasmi ya utambuzi kutoka chuo hicho.

Zaidi ya hilo, Kang’ethe sasa anasema amekuwa nabii aliyetwikwa jukumu jingine la kukiokoa kizazi kilichopotea kwa kuliletea taifa ujumbe kutoka kwa Mungu hasa wakati huu nchi inapoelekea kwenye uchaguzi.

“Nilikuwa nimelala nilipopata ujumbe huu kwenye ndoto” anasema kuwa kwanza alilichukulia kama jambo la mzaha lakini ilipotokea mara ya pili ilibidi atii na awasilishe ujumbe.

Kwenye ujumbe Kang’ethe anaosema alipokezwa anashauri kuwa siku za mwisho zimekaribia na kuwa wakati wa Mungu kuvuna umewadia.

Kangethe anaonya kuwa kuwa kwenye ndoto yake aliona majanga matatu yenye nguvu na kasi nyingi kuliko Covid-19 ila watakaopona ni wale ambao wale njia zao ni nyoofu.

Nabii huyu anasema kuwa kuna uwezekano wa kutokea vurugu za kidini ila hili linaweza kukabiliwa na kuepukika ikiwa dini zitakubaliana kuwa zinamwabudu mungu mmoja.

Kangethe anasema aliokolewa kutokana na minyororo ya wabudu shetani chini ya uongozi wa mwanamke mmoja Jezebeli ambaye alitaka kuinyakua roho yake ila msingi wake wa kidini ulimlinda.

Kwa sasa ana imani kuwa ujumbe huu alioupata na kuuwasilisha kwa viongozi tajika wa kisiasa na kidini na watu wengine utakumbatiwa na kufanyiwa kazi.

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.