Mauaji ya wakongwe: Kimya cha viongozi huchangia kuuawa kwa wazee

Wiki iliyopita video ya watu waliokuwa wanajiyatarisha kumuua mkongwe mmoja huko eneo la Kisii ilienea mtandaoni.

Kulingana na picha hiyo, maskini mwenye umri wa miaka 85 alizungukwa na kundi la watu ambalo walimpiga na kisha kumchoma hadi kufa kwa kile kinachodaiwa ni kuwa uchawi.

Kwa ukweli hakuna kitu kinachosikitisha kama kuona wakongwe ama mtu yeyote yule akiuawa. Kwanza bila wakongwe hakuna kizazi cha sasa na inauma kuona kizazi hiki kikigeuka asili yake  kwa sababu ya mtu amekuwa mkongwe na amejawa na mvi kichwani.

Mara nyingi wanaochangia kuuawa kwa wakongwe hao huwa ni jamaa na familia ya anayeshukiwa kuwa mchawi

Tabia na hulka za jamii kuwaua wakongwe zimeenea sana katika maeneo ya pwani na kaunti za Kisii na Nyamira licha ya kuwa katiba inamhakikishia kila mkenya haki yake ya kuishi.

Mauaji bila kutekeleza haki

Wanaotekeleza maovu haya hujifanya kuwa ni washtaki, watetezi na waamuzi na hivyo kukamilisha  kesi hizo katika muda mchache zaidi huku anayeshtakiwa akikosa kupewa fursa ya kujitetea na hata kama angejitetea hangesikilizwa.

Linalosikitisha zaidi ni kuwa baadhi ya viongozi na hasa wanasiasa walioko kwenye nyadhifa na hata wale wanaowania huunga mkono harakati za kuwaua wakongwe kwa sababu za kisisiasa

Aidha hawataki kuonekana kama ambao wanapinga tamaduni hizo potovu kwa sababu ya hofu kuwa huenda wakapoteza nafasi zao za kisiasa ama wakakosa kuchaguliwa.

Wanasiasa hao mbao wengi wao ni wasomi na watu waliostaarabika hasa kutokana na kuingiliana na watu wengine nchini na hata katika mataifa ya kigeni hufyata midomo na kuangalia tu ka mbali maovu yakitendeka.

Viongozi huchangia mauaji

Wakati mwingine wanasiasa hao hata huchangia katika kuwalipia washukiwa dhamana na hatya kuwalipia mawakili ili waachiliwe kutoka korokoroni na wanasiasa husika wapate umaarufu.

Kwa upande mwingine wazee wa mitaa na maafisa wa ngazi za chini serikalini pia huweka kimya cha maji mtungini na kujitia hamnzao kwa sababu kimoyomoyo wao ni washirika wa tamaduni husika na hivyo wanaunga mkono tabia hizo na hawataki kuonekana kama ambao wanaenda kinyume nazo.

Kuna haja ya kuweka sheria kali ambayo itazuia mtu yeyote kumutoa mwingine uhai hasa kutokana na tuhuma za kichawi. Pili mashirika ya kijamii yanafaa kuingilia kati na kuwaelimisha watu wa jamii husika kuhusiana na athari za kuwatoa wazee uhai kwa familia, jamii nan chi nzima kwa jumla.

Zaidi wabunge hasa kutoka sehemu ambazo visa hivi hutokea ama mbunge yeyote yule anayeali uhai wa mkongwe wana jukumu la kuimarisha sera itakayohakikisha wakongwe wanalindwa.  

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.