Mapenzi Kibao: Kina baba wakiuka utamaduni kwa kuwalea watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza umri

Mapenzi Kibao: Kina baba wakiuka utamaduni kwa kuwalea watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza umri

Na Victor Moturi

Ni tarajio la kila mama mja mzito kuwa atajifungua salama na katika wakati unaotarajiwa.
Lakini si kila mara mambo huenda kwa mpango na wakati mwingine mtoto huzaliwa kabla ya umri kutimia. Ila swala ni je ni vipi watalelewa hadi watimize uzani unaoendana na umri wa kuzaliwa
Mojawapo wa mbinu za kuwakuza watoto wanaozaliwa kabla ya umri kutimia ni ile ya “Kangaroo mother care” ambayo inahusisha kumueka mtoto kifuani hadi uzani wake uongezeke.
Humu nchini Kenya mbinu hii ambayo iliasisiwa nchini Malawi imeshika kasi na hata kukubalika miongoni mwa baadhi ya wanaume ambao sasa wanawasaidia wake zao kuwalea watoto hao hadi watimize uzani hitajika.
Mbinu hii humuwezesha mama kumfunga mtoto kifuani, na kumsaidia kupata joto kama ile ya nasari, ili mtoto kuongeza uzani kwa haraka na hutumika kwenye hospitali zilizo na uhaba wa nasari.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa mifumo mingi ya afya barani Afrika ikiwemo Kenya, imekumbwa na changamoto kama vile ukosefu wa umeme pamoja na barabara mbovu ambazo huchangia akina mama wengi kutoenda hospitalini kujifungua, hali ambayo husababisha watoto wengi kufariki kutokana na ukosefu wa nasari katika hospitali mbalimbali hasa mashinani.

Kukiuka utamaduni

Baba amsaidia mkewe kumlea mtoto hadi umri wa kuzaliwau utimie

Lakini sasa, kina baba maeneo ya magharibi mwa Kenya wamekaidi utamaduni na sasa wanawasidia akina mama kupeana huduma hii ya kangaroo hospitalini na hata nyumbani.
Chukua mfano wa Jackton Makwata, mumewe Anita ambaye alienda hospitalini kumsaidia mkewe kumlea mtoto wao ili atimize uzani hitajika.
“Nilikuja kumsaidia mama kukangaroo huyu mtoto. Ninafurahja kwa sababu hii kazi si rahisi na si wengi wanaitikia lakini mimi nilijitolea kwa hivyo kufika mahali tumefikia nina furaha kuwa uzani wa mtoto umeongezeka,” akasema Makwata.
Makwata anasema licha ya kuwa kuna wale walimcheka alianya hivyo kutokana na mapenzi ya mtoto na mama yake.
Kulingana na takwimu, hospitali ya Webuye ni mojawapo ya hospitali magharibi mwa Kenya ambazo zinarekodi idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wao.
Kwa mujibu wa muuguzi Grace Oniang’o wengi wa kina mama huchoka sana na hivyo wanahitaji kusaidiwa, na ni jambo nzuri kuona wanaume wakijitokeza kuwasaidia.
Hata hivyo kuna baadhi ya watu ambao wanaona kuwa wanaume hao wamekiuka tamaduni na maadili huku wakisema kazi ya kulea watoto ni ya kina mama.
“Baadhi ya wanaume wanachukulia jambo la kangaroo ama kulea mtoto ni la mama, si la baba. Sasa wakati wanakuona ukifanya kazi kama hiyo, wanaona kana kwamba mama amekukalia” anasema Philip Barasa ambaye anamsaidia mkewe kumuangalia mtoto wao nyumbani.

Kuokoa maisha ya watoto

Tangu mpango huu wa kangaroo kuanzishwa nchini miaka tisa iliyopita, mataifa Jirani kama vile Uganda na Tanzania, pia yamejitosa ndani ili kuyaokoa maisha ya maelfu ya watoto.
Mataifa mengine ambayo pia yanaangazia kangaroo ni kama vile Rwanda, visiwa vya Comoro, Nigeria, Togo, Mali na Niger.
Wataalam kutoka Shirika la Save the Children wanashauri kuwa mtoto anapokuwa chini ya mpango wa kangaroo, huwa na akili ya hali ya juu maarufu IQ.
Kulingana na Shirika la Save the children, takriban watoto 9,000 wamenufaika na mpango huu humu nchini.

Victor Moturi ni mwandishi mahiri kutoka mjini Nairobi ambaye ameshinda tuzo kadhaa kutokana na taarifa anazoandika kuhusu afya na kilimo katika eneo la Afrika Mashariki

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.