Ligi ya KPL yaregea, Timu kongwe zaonyeshwa cha mtema kuni

Ligi ya KPL yaregea, Timu kongwe zaonyeshwa cha mtema kuni

Na Edwin Muthomi

Baada ya kusimamishwa kwa takriban wiki tatu, ligi kuu nchini KPL imerejea kwa mpigo huku timu kongwe zikikosewa heshima na timu zinazoibuka.

Kariobangi Sharks imeinyuka City Stars mabao 2 kwa 1 huku Sofapaka ikiiweka polisi korokoroni kwa kuizaba mabao 2 bila jibu.

Wazito nayo imebomoa ngome ya Ulinzi kwa kuwapiga risasi moja ya moto huku nayo Bidco nayo ikiirarua Ingwe AFC Leopards bao moja bila jibu. Vijana wa mabanda Mathare United wamenyamazishwa kwa kulishwa mawili makavu na Talanta FC huku Kakamega Homeboyz ikinywa sukari ya Nzoia Sugar bao moja kwa nunge.

Michezo hiyo imeregea wiki tatu baada ya Waziri wa mchezo na utamaduni Balozi Amina Mohamed kutupilia mbali shirikisho la soka nchini FKF kwa tuhuma za ufisadi.

Rais wa shirikisho hilo Nick Mwendwa alitiwa mbaroni mara mbili na kisha baadaye kujiuzulu kama wenyekiti.

Kwa sasa ligi inasimamiwa na kamati shikilizi chini ya uongozi wake Jaji Mstaafu Aaron Ringera inapania kuchukua mwelekeo mpya licha ya changamoto zinazovikumba vilabu vya soka nchini Kenya.

Aidha kabla ya kuanza rasmi, kamati hii imeahidi vilabu pamoja na marefarii wa viwango vyote nchini ufadhili kifedha na malipo ya mapema ikiwa ni baadhi ya matatizo yaliyokuwa yakikumba sekta hii ya soka.


Mechi ya siku ya jumapili itakuwa moja, ugani utalii ambapo wanabenki KCB watakuwa wakipania kuwapa mkopo wa mabao Vihiga Bullets wanaoshikilia mkia ligini kwa alama moja peke yake.


Edwin Muthomi ni mwandishi wa Habari anayeibuka na anayependa kuandika taarifa za michezo, ulibwende na biashara. Anapatikana kupitia barua pepe gurusomi18@gmail.com

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.