Kuku wanaumia, tamaa ya kuku na mayai yapelekea ukiukaji wa haki za kuku

Kuku wanaumia, tamaa ya kuku na mayai yapelekea ukiukaji wa haki za kuku

Na Victor Moturi

This image has an empty alt attribute; its file name is PHOTO-POULTRY-IN-CAGES-2-1024x620.jpg
Kuku wanaozuiliwa kwenye cage. Wataalam wanasema haki za msingi za wanyama hawa zinakiukwa. Picha: Victor Moturi

Katika siku za hivi karibuni, wakulima wengi wa kuku wamezingatia kilimo cha kuku wa kufungia kwenye cage kutokana na uhitaji mkubwa wa mayai, uhaba wa ardhi, na kama njia ya kuzuilia migogoro kati ya binadamu na wanyama kuhusu uharibifu wa mimea

Mashirika ya haki za wanyama yanasema kilimo hicho kinakiuka haki za wanyama kwa kuwazuilia mahali padogo ambapo haki zao hazikuzingatiwa.

Hata hivyo Stella Njoroge ambaye ni mkulima wa kuku katika eneo la Kikuyu kaunti ya Kiambu anasema kuwa kilimo cha kuku wa kufungia ni kizuri kwani kinafanya udhibiti wa kuku kuwa urahisi.

“Kwa sasa napata mayai zaidi kuliko vile nilivyokuwa napata kwa kuku wa kuachilia. Naweza hata pata trei sabini za mayai kwa siku,” anasema Njoroge.

Ukulima wa kuku ni muhimu kwenye uchumi kutokana na mahitaji makubwa ya nyama na mayai, chanzo cha ajira na kadhalika na wakulima wengi wanatumia mbinu tofauti tofauti kuimarisha mapato yao.
Kwa baadhi ya wanununzi, mayai kutoka kwa kuku wa kufungia kwenye cage ni mazuri zaidi.

“Wateja wangu husema mayai haya ni masafi na laini na nina watu wengi ambao kwa sasa wananinunulia,” anasema Judy Kinoti mmoja wa wateja wa Bi. Njoroge.

Uhaba wa ardhi, mivutano na gharama ya madawa ni mojawapo wa mambo yanayowafanya wakulima wengi kuzingatia kilimo cha kuku wa kufungia.

“Kilimo hiki pia kinasaidia katika kupunguza visa vya wizi wa kuku,” anasema Peter Kinyua kutoka sehemu ya Kamigumo Kaunti ya Kiambu.

“Kufungia kuku hivi ni vizuri kwa sababu hawawezi kupata magonjwa huku nje, halafu wakati kuku wanarandaranda huko nje kuna wanyama wengine wanaweza kuwala, wanaweza ibiwa, na pia huwezi ukajua kuku wanataga wangapi,” anasema Kinyua
Lakini kwa mujibu wa mashirika ya haki za wanyama kilimo aina hii kinakiuka haki za kuku kwa kuwapunguzia uhuru wao.

This image has an empty alt attribute; its file name is PHOTO-POULTRY-IN-DEEP-LITTER-SYSTEM-1-1024x529.jpg
Kuku wanaoutunzwa katika sehemu za wazi. Hili huwawezesha kuwa na uhuru wa kutembea na hata kujiosha. Picha: Victor Moturi

Daktari Victor Yamo mtaalamu wa haki za wanyama anasema kilimo hiki kinakiuka haki msingi za tano za wanyama vile kukiuka uhuru dhidi ya mateso, uhuru wa kuwa na tabia asili, kukosa mahali kwa kutaga na hata kughafilika kila wakati yai linatagwa.

“Mfumo huu huleta magonwa kwa kuku, humfanya kuku kusimama muda mrefu kwenye waya na hana nafasi ya kupumzika hivyo kumuacha akiwa na vidonda vingi kwenye miguu. Kuku hana uhuru wa kufanya mazoezi na pia hapati jua la kutosha.” Yamo ambaye ni afisa katika Shirika la kulinda haki za wanyama ulimwenguni anasema
Yamo anaongezea kuwa humu nchini hakuna mifumo madhubuti ya kisheria ama sera ambayo itasaidia kuimarisha haki za kuku.

“Mfumo huu umepigwa marufuku katika nchi za bara Uropa,” anasema Yamo huku akiongeza kuwa nchi nyingi zinazingatia mfumo wa kuweka kuku katika sehemu wazi ambazo zina nafasi ya kutosha kuwawezesha kuku kukimbia, kucheza na hata kujiosha.

Mfumo huo pia husababisha kuku kuwa na mifupa dhaifu kwa sababu hazina nafasi ya kutoka nje. Hata hivyo kulingana na Njoroge, yeye huwaachilia kuku wake mara kwa mara watoke nje wapate nafasi ya kukimbia na kupata jua.

Licha ya mchango mkubwa wakulima wa kuku wanaofanya kwa uchumi wa taifa, hakuna sheria hata moja ambayo inayoangazia kilimo cha kuku.

Hata hivyo kuna miswada kadhaa bungeni kuhusu wanyama ambayo inangojea kujadiliwa na kufanywa sheria.
Wakulima wa kuku wanasema wataendelea kuzingatia kilimo hiki licha ya mashirika ya haki za wanyama kusema kunahitajika suluhu kuhusu na kuangazia kilimo ambacho hakikiuki haki za wanyama.

Victor Moturi ni mwandishi mahiri kutoka mjini Nairobi ambaye ameshinda tuzo kadhaa kutokana na taarifa anazoandika kuhusu afya na kilimo katika eneo la Afrika Mashariki


admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.