Je, wimbi la Sonko litatifua Ugavana Mombasa?

Je, wimbi la Sonko litatifua Ugavana Mombasa?

Asiye na mja ana mola, ndio kauli ya wapiga kura wengi wa Mombasa ambao walikuwa wanamuunga mkono mgombea ugavana kwa tiketi ya ODM Suleiman Shahbal ambaye aliachilia mikoba bila ilani.

Wengi wa wafuasi hao walibubujikwa machozi michirizi michirizi baada ya kufahamishwa kuhusu kauli hiyo huku wakiachwa hoi wasijue pa kwenda. Baadhi ya wadadisi wanadai wafuasi hao walikuwa wanalia hasa baada ya kuona mfereji ikikauka maji mbele ya macho yao tena mchana peupe.

Sonko awazungumzia wafuasi wake muda mfupi baada ya kuidhinishwa na mahakama. Picha: Mike Sonko

Hata hivyo machozi yao ya uyatima wa kisiasa yalipanguzwa siku chache baadaye baada ya aliyekuwa gavana wa Nairobi aliyeng’atuliwa Mike Sonko kutangaza kuwania ugavana kwa tiketi ya chama cha Wiper kilichoko kwenye Muungano wa Azimio unaoongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga.

Lakini Sonko alikabiliwa na vizuizi chungu nzima na baada ya kung’ang’a na kesi mahakakani hatimaye aliruka vizuizi kadhaa na kuruhusiwa kuwania ugavana wa Mombasa, Jumatano iliyopita, huku baadhi ya wafuasi wake wakiangua kilio cha furaha kutokana na hatua hiyo.


Hatua hiyo imeshangiliwa na wafuasi wake ambao wanamsifu Sonko kwa kile wanachosema ni uwezo wake wa kulifungua pochi na kuachilia.


“Mkono wake unakunjuka vilivyo na anawasadia watu pasipo kuangalia dini wala kabila,” akasikika akisema Mama Khadija mwenye asili ya Kiswahili na mfuasi sugu wa Sonko.


Namuombea dua kila asubuhi ili Mwenyezi Mungu amuondolee vikwazo na aweze kuongoza mji wetu akasema mkazi huyu wa mji wa Kale wa Mombasa.


Hata hivyo kuidhinishwa kwa Sonko kumeutia tumbo joto upande wa Azimio hasa kwa vile anaonekana kama ambaye amekuja kugawanya kura.

Sonko akabidhiwa cheti cha kuwania ugavana Mombasa. Picha: Mike Sonko


Baadhi ya wadadisi wanasema huenda Hassan Omar wa Chama cha UDA akapita katikati ya Sonko na Abdulswamad Sheriff Nassir wa ODM. Kwa wengi hata hivyo Hassan Omar bado hajakuwa na mvuto unaohitajika kumwangusha Abdulswamad na kwa hivyo kinyang’anyiro kitakuwa kati ya Abdulswamad na Sonko.


Sonko pia anaogopewa kwa sababu ya uwezo wake wa kuwakusanya wafuasi hasa wale ambao ni maskini na hufurahishwa na vitendo vyake vya kutoa fedha na misaada mingineo.

Sonko akiwa na mgombea mwenza wa kiti cha ugavana Mombasa Ali Menza Mbogo. Picha: Mike Sonko


Aidha kuidhinishwa kwa Sonko kumezua migawanyiko huku baadhi ya watu wakisema kuwa Sonko hafai kuchaguliwa Mombasa kwani huo ni mji wa waswahili na unastahili kuongozwa na waswahili pekee.

Kwa baadhi ya watu Sonko pia alishindwa kuungoza mji wa Nairobi na hawaoni ni kwa njia gani ataweza kuongoza Mombasa.

Watetezi wake hata hivyo wanasema hakushindwa kuongoza mji mbali baadhi ya wakuu wa serikali walikuwa hawamtaki kutokana na kile kinachosemekana ni sababu zao za kibinafsi.

Swali linalowakuna wengi vichwa ni je? Mawimbi ya Sonko yatatikisa kwa kiwango gani mji wa Mombasa?

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published.